Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wachezaji watano wa timu ya
Rusumo FC ya mkoani Kagera vilivyotokea jana jioni mkoani humo
Rusumo FC ilikuwa ikitoka kwenye
mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani kurudi
Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano kufariki
papo hapo.
Wachezaji wengine ambao ni majeruhi
wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao
zikiwa mbaya.
Msiba huo ni pigo kwa familia za
marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA),
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya soka nchini
kutokana na mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa mchezo huu kupitia klabu
yao.
TFF inatoa pole kwa familia za
marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Kutokana na msiba huo, mechi zote za
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania zinazochezwa leo zimekuwa na dakika moja ya
maombolezo ili kutoa heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za marehemu
mahali pema peponi. Amina
0 comments:
Post a Comment