SIMBA YAPOKEA KWA MASIKITIKO MSIBA WA MWAIMU.



KLABU ya soka ya Simba imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Katibu Mwenezi wake wa zamani, Robert Charles Sechawawa Mwaimu, kilichotokea juzi Jumanne nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa SIMBA, Geofrey Nyange Kaburu, kwa niaba ya uongozi wa Simba amesema msiba huo umeleta pengo kubwa kwa klabu hiyo kutokana kuendelea kuhitajika kwa  mchango wake.

Mwaimu alikuwa Katibu Mwenezi wa Simba mwishoni mwa miaka ya 1990 wakati Simba ikiwa chini ya uenyekiti wa Yusuf Hazali na Katibu Mkuu akiwa Halfani Mazi Matumla.

Zaidi ya Simba SC, Mwaimu alipata kuwa mfanyakazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mamlaka ya Mkonge Tanzania kabla ya kwenda Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) alikokuwa akifanya kazi hadi wakati anaanza kuwa Katibu Mwenezi wa Simba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia ya Mwaimu, marehemu atazikwa kesho Ijumaa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam majira ya saa 9:30 alasiri.

Shughuli zote za ibada ya mazishi zitafanyika nyumbani kwa marehemu, Kenyatta Drive Namba 22, Oysterbay kuanzia saa tano asubuhi.

Mola na ailaze roho ya marehemu mahali pema. Amina

0 comments:

Post a Comment