USAJILI/PINGAMIZI DHIDI YA WACHEZAJI
Musa Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji Musa Hassan Mgosi ameombewa
usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya
Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
Toto dhidi ya Kagera Sugar kumsaini
Enyinna Darlinton Ariwodo
Toto Africans ilipinga usajili wa
Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile bado ina mkataba wa
mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa upande wake Kagera Sugar ilisema
imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa kumlipa mshahara
ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo ikishindwa kumlipa
mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni
mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa kutimiza
masharti ya mkataba.
Ramadhan Chombo ‘Redondo’
Redondo ameidhinishwa kuchezea Simba
kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana (Fair Play) baada ya klabu hiyo na
ile ya Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.
Mchezaji David Luhende kusajiliwa Yanga
Yanga ilikiri kutolipa ada ya uhamisho
ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana na Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera
Sugar hundi iliyogonga mwamba benki (bounced cheque). Shauri hilo lilimalizwa
kwa Yanga imetakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia Septemba 10
mwaka huu.
Super Falcon dhidi ya Edward
Christopher kusaini Simba
Simba imepewa siku 21 kuanzia Septemba
10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo (compensation) kwa vile
ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
Toto Africans dhidi ya Mohamed Soud
kusajiliwa Coastal Union
Toto Africans iliweka pingamizi kwa
maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi wa Fair Play,
mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono kati ya klabu.
Rollingstone dhidi ya Kigi Makassy
kusajiliwa Simba
Simba imetakiwa kuilipa Rollingstone
gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na mchezaji huyo kwa kuzingatia
kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Super Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija
kusajiliwa Coastal Union
Uamuzi wa Kamati ni kuwa Shija
atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 23, Coastal
Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia kumhudumia mchezaji huyo.
African Lyon dhidi ya Razak Khalfan
kusaini Coastal
Lyon imesema bado ina mkataba na
mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Lyon
umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union.
Flamingo dhidi ya Kelvin Friday
kusajiliwa Azam
Friday ruksa kucheza Azam, lakini klabu
hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu kuilipa Flamingo gharama za
kuvunja mkataba.
Super Falcon dhidi ya Robert Joseph
Mkhotya kusaini African Lyon
Lyon imeagizwa kuilipa Super Falcon sh.
milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ambaye
imemsajili. Fedha hizo zitalipwa kwa awamu nne kutokana na makato ya mlango
yatakayofanywa na TFF. Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF.
Oljoro JKT dhidi ya Othman Hassan
kusajiliwa Coastal
Kwa mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa
mchezaji huyo na Oljoro JKT unamalizika mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni
mchezaji halali wa Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.
Yanga dhidi ya Simba kuacha wachezaji
wanne
Kamati imetupa pingamizi hizo kwa vile
hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji juu ya kuvunjiwa mikataba yao.
Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga
na Lino Masombo.
Ikiwa wachezaji hao watakuwa na
malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo litafikishwa katika Kamati kwa
ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mbuyu Twite
Kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni
za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali. Hata hivyo,
kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na
kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku
21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Kelvin Yondani
Kwa mujibu wa Ibara ya 44(3) ya Kanuni
za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili
Kelvin Yondani, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo
vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine
kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria
kwa mujibu wa madai/lalamiko husika.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji
0 comments:
Post a Comment