Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Oktoba 11,
2012 kujadili michakato ya chaguzi mbalimbali za wanachama wa Shirikisho.
Katika kikao chake, Kamati ilijadili michakato ya chaguzi za viongozi wa Chama
cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Chama cha Waamuzi wa Mpira wa
Miguu (FRAT), Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama
cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es salaam (DRFA),.
Pia
Kamati ilijadili mchakato wa chaguzi za Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA)
na kupokea mchakato wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Mbeya (MRFA).
Baada
ya kujadili chaguzi hizo kwa kina, Kamati ilifikia uamuzi ufuatao:
1. FRAT
Uchaguzi wa FRAT haukufanyika baada ya
wajumbe kugoma wakipinga kuondolewa kwa baadhi ya wagombea. Kamati ilikubaliana
kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya FRAT kuhakikisha uchaguzi unafanyika Novemba 17,
2012 na kufanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na sehemu ambako
uchaguzi huo utafanyika. Mkutano utatakiwa kuwapigia kura wajumbe waliopitishwa
kugombea uongozi tu.
2. RUREFA
Baada ya kufuta uchaguzi wa viongozi wa
RUREFA na kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
imeitaka Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuteua kamati mpya ya uchaguzi ya chama
hicho kabla ya Oktoba 20, 2012 na kuiagiza kamati mpya kuwa imeshatangaza
mchakato wa uchaguzi ifikapo Oktoba 24, 2012.
3. SHIREFA
Kamati ilipokea pingamizi dhidi ya
baadhi ya wagombea uongozi wa SHIREFA na hivyo kuagiza walioweka pingamizi na
waliowekewa pingamizi pamoja na mwakilishi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA
kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Alhamisi ya
Oktoba 18, 2012 kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.
4. MRFA
Kamati
ilipokea rufaa na pingamizi kutoka kwa baadhi ya wagombea walioenguliwa kuwania
uongozi wa chama hicho na hivyo imewataka walioweka pingamizi na waliokata
rufaa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Oktoba
18, 2012 jijini Dar es salaam.
5. TASMA
Kamati iliona mapungufu katika mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa TASMA na kuamua chama hicho kifanye uchaguzi ifikapo
Desemba mosi badala ya uchaguzi kufanyika Oktoba 27, 2012 kama ilivyokuwa
imepangwa awali. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya
TASMA kuhakikisha kasoro zilizojitokeza zinarekebishwa ili uchaguzi ufanyike
kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na Kanuni za Uchaguzi.
6. DRFA
Awali,
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilitangaza kuwa hatma ya uchaguzi wa DRFA itajulikana
baada ya kikao cha leo, lakini kutokana na wajumbe kutoweza kuhudhuria kwa
sababu tofauti, mustakabali wa suala hilo sasa utajulikana baada ya kikao cha
Oktoba 18, 2012.
Wagombea
na wadau wanaotakiwa kuhudhuria kikao cha Oktoba 18, 2012 wanataarifiwa kuwa
kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za TFF kuanzia saa
08:2012.
Kamati
inawaomba wajumbe wote kuhudhuria bila ya kukosa.
Angetile
Osiah
Katibu
Mkuu TFF
0 comments:
Post a Comment