CHAMA cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA), kimesikitishwa na taarifa za baadhi ya
waandishi wa habari za michezo kupewa vitisho wanapokuwa wanatekeleza majukumu
yao ya kazi.
Katibu mkuu wa TASWA Amiri Mhando amesema kuwa uongozi umepokea
malalamiko kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari za michezo wakidai
baadhi ya wanachama wa Yanga a.k.a ‘Makomandoo’ wamewapa vitisho kabla na
baada ya mchezo kati ya Kagera Sugar na Yanga uliofanyika Jumatatu wiki hii
Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
Sekreterieti ya TASWA ilifanya
mawasiliano ya haraka na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Onesmo Kapinga ambaye
alikuwa mkoani Kagera na amethibitisha pasi na chembe ya shaka kwamba vitisho
hivyo vimewanyima fursa ya kutekeleza majukumy yao ya kazi.
Tukio hili limetuhuzunisha sana kwa
sababu licha ya kuwajengea hofu baadhi ya waandishi wa habari kushindwa
kutekeleza majukumu yao ya kazi kikamilifu, lakini linaweza kujenga chuki
zisizo na msingi kati ya klabu hiyo na TASWA.
Wanachama na mashabiki wa klabu
kubwa hapa nchini Simba na Yanga wakubali changamoto za viwanjani na wasitake
kutafuta mahali pa kupeleka lawama zao pale wanapoona matokeo mabaya kwa klabu
zao.
Si nia ya TASWA kutetea udhaifu kama
upo kwa baadhi ya waandishi wa habari, lakini tunaona kwa malalamiko
yanayotolewa na baadhi ya makomandoo hao kwa wanahabari si mazuri na hoja zao
hazina mashiko ni kutapatapa.
Tunauomba uongozi wa Yanga uwakemee
mashabiki wake waachane na mambo yasiyo na msingi ambayo hayana manufaa kwa
klabu hiyo na ulimwengu wa soka hapa nchini. TASWA inataka wanahabari wawe huru
kutekeleza majukumu yao na hilo tuna hakika litafanyika.
Kamati ya Utendaji ya TASWA
inatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki ijayo kujadili suala hili la vitisho kwa
wanahabari na pia itajadili masuala mbalimbali ikiwemo kutaja mkoa
utakakofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama.
0 comments:
Post a Comment