
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26
mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa
katika viwanja sita tofauti.
Mabingwa watetezi Simba
watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha
Simba tangu kiliporejea kutoka Oman kwenye ziara ya mafunzo.
Pia Kocha wake mpya,
Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho
katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses Basena na Jamhuri Kihwelo.
Mwamuzi wa kimataifa Israel
Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo African Lyon inatarajiwa
kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya kusitisha kibarua cha Pablo Velez
kutoka Argentina kutokana na kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza.
Uwanja wa Manungu ulioko
Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo
utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji Mtibwa
Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL ililazimisha
suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Coastal Union ambayo kwenye
dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo Mzimbabwe Tinashe Machemedze
itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa
Mkwakwani, jijini Tanga.
Timu zinazo katikati ya
msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa
Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa
miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Wawakilishi wa Tanzania
kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za kirafiki nchini
Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya
Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ni mechi ya kulipa kisasi
kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza
iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Maafande wa Oljoro JKT
wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto
Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid,
jijini Arusha.
0 comments:
Post a Comment