Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeahirisha uchaguzi wa Chama cha Makocha wa
Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliokuwa ufanyike leo (Januari 19 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam.
Uchaguzi umeahirishwa kwa vile
ulitaka kufanyika bila kuzingatia Katiba ya TAFCA Ibara ya 32(1) na Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6) na 26(2), hivyo Kamati ya Uchaguzi
ya TFF imeahirisha uchaguzi huo kwa vile nafasi zilizoombwa kugombewa na idadi
ya waombaji uongozi haikidhi matakwa ya Katiba ya TAFCA.
Pia taratibu za kikanuni ikiwa ni
pamoja na kuwaarifu waombaji uongozi ambao hawakukidhi matakwa ya Katiba ya
TAFCA hazikukamilika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Licha ya upungufu huo, TAFCA
haikuwasilisha taarifa za mchakato mzima kama ilivyoombwa na TFF. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA kuandaa uchaguzi mpya
utakaokidhi matakwa ya Kamati ya TAFCA baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF.
TFF inaishauri TAFCA kutumia
fursa ya Mkutano Mkuu wa leo (Januari 19 mwaka huu) kujadili mustakabali wa
TAFCA kwa kuwa chama hicho kimeshindwa mara mbili kupata idadi ya wagombea
wanaokidhi akidi ya Kamati ya Utendaji.
Pia TAFCA haijawahi kufanya
mikutano ya Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu kwa karibu miaka minne.
0 comments:
Post a Comment