Wakati mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza Jumamosi (Januari
22 mwaka huu), mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) umesogezwa mbele
kwa wiki moja ambapo sasa utaanza Februari 2 mwaka huu.
Uamuzi wa VPL kuendelea Januari
26 mwaka huu ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu za ligi hiyo kilichofanyika jana (Januari 21
mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, uamuzi huo umefikiwa
huku yakiwepo masharti kadhaa kutokana na uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kukamata sh. milioni 157 kwenye akaunti za TFF, fedha ambazo zilitoka kwa
mdhamini wa VPL (Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom) kwa ajili ya timu
zinazoshiriki ligi hiyo.
Masharti hayo yatawasilishwa na
Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), nakala kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Awali klabu kupitia Kamati ya Ligi zilisisitiza zisingecheza ligi hadi fedha
hizo zitakaporejeshwa.
Kwa upande wa FDL itaanza bila
timu ya Small Kids ya Rukwa ambayo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada
ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi
hiyo, matokeo yote ya mechi ambazo Small Kids ilicheza katika mzunguko huo wa
kwanza yamefutwa.
0 comments:
Post a Comment