NYAMLANI ATEULIWA KAMATI YA AFCON
2013
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani ameteuliwa kuwemo
kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) utakaosimamia
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani
nchini Afrika Kusini.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa
CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo wa CAF kwa ajili ya
fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu una
jumla ya watu 148.
Nyamlani ni mmoja wa wajumbe
watatu watakaoshughulikia masuala ya rufani. Wajumbe wengine ni Prosper Abega
kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon. Nyamlani ni mjumbe wa Bodi
ya Rufani ya CAF yenye watu 12.
SERENGETI BOYS YAINGIZA MIL 23/=
Mechi ya mchujo ya Kombe la
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti
Boys) na Congo Brazzaville iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
imeingiza sh. 23,021,000.
Kwa mujibu wa msemaji wa TFF
Boniface Wambura amesema mapato hayo yametokana na washabiki 18,022 waliokata
tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 10,000, sh. 5,000, sh.
2,000 na sh. 1,000. Washabiki 15,850 walikata tiketi za sh. 1,000.
Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo
ni sh. 3,511,677.97 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati
gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 5,956,635), usafi na ulinzi (sh.
2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh. 400,000), Wachina-
Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na ulinzi wa mechi
(sh. 3,500,000).
Kwa upande wa mgawo asilimia 20
ya gharama za mechi ni sh. 1,000,537, asilimia 10 ya uwanja sh. 500,269,
asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 250,134, asilimia
45 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,251,209, asilimia 20 ya
TFF (sh. 1,000,537) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 50,027.
UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA
MIGUU MKOA WA KATAVI (KAREFA)
Mchakato wa uchaguzi wa KAREFA
umefutwa kutokana na wagombea watano kati ya nane vyeti vyao vya elimu ya
sekondari kuwa na utata. Mchakato wa uchaguzi huo utaanza upya Novemba 21 mwaka
huu.
UCHAGUZI WA TASMA
Mchakato wa uchaguzi wa Chama cha
Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utaanza upya Novemba 26 mwaka huu
baada ya mchakto wa sasa kupata wagombea kwenye nafasi mbili tu za Kamati ya
Utendaji ya chama hicho.
UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA
MIGUU MKOA WA RUKWA (RUREFA)
Mchakato wa uchaguzi wa RUREFA
utaanza Novemba 26 mwaka huu na Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA itapewa maelekezo
ya usimamiaji wa uchaguzi huo baada ya mchakato wa awali kuwa umefutwa kutokana
na kufanyika bila kuzingatia kanuni za uchaguzi.
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika
keshokutwa (Novemba 22 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 6 kamili mchana
kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
0 comments:
Post a Comment