Timu ya Ruvuma imethibitisha kuwa mwiba mkali katika michuano ya Copa Coca-Cola mwaka huu baada ya leo asubuhi (Julai 2 mwaka huu) kuishushia Lindi kipigo cha mabao 7-2.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani, washindi ambao kwa matokeo hayo wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Waliotikisa nyavu ni Anthony Christian dakika ya 23 na 50, Edward Songo dakika ya 27, 75 na 86 na Sunday Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao ya Lindi yalifungwa na Salum Mnyamwile dakika ya 18 kwa njia ya penalti na lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami Maundu.
Nayo Tanga imepata ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kuifunga Manyara mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60.
0 comments:
Post a Comment