KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Idd Mtiginjola imetupa maombi ya kufanyia
marejeo (review) uamuzi wake kama yalivyowasilishwa mbele yake na waombaji
watano.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za
TFF, Dar es Salaam leo mchana (Februari 18 mwaka huu), Mtiginjola ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema wamepitia Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi
za TFF na kubaini kuwa hakuna Ibara yoyote inayotoa fursa ya review kwa uamuzi
ambao wameshaufanya.
Amesema Kanuni za Mwenendo wa Madai (CPC) katika
mahakama za kawaida zinaruhusu Hakimu aliyefanya uamuzi katika kesi kufanya
marejeo, lakini katika masuala ya mpira wa miguu hakuna fursa hiyo, hivyo
hawawezi kujitungia kitu kipya kwani kazi yao ni kufanya uamuzi kwa kutafsiri
Katiba na kanuni walizopewa na mamlaka ya uteuzi (TFF).
Waombaji watano waliokuwa wakitaka Kamati hiyo ifanyie
marejeo uamuzi wake kutupa rufani zao ni Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa
kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha
kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine ambao waliomba kuwania ujumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano ni Eliud Peter Mvella (Iringa na
Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na
Simiyu).
0 comments:
Post a Comment