SHIRIKISHO la Kimaifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo mchana (Februari 19 mwaka
huu), Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato
wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko.
Amesema kutokana na mkanganyiko
huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka huu- imeambatanishwa)
imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika Februari 24
mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake nchini.
Ujumbe huo wa FIFA unatarajiwa
kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo utafanya tathimini ya hali
hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na baadaye kutoa mwongozo wa
nini kifanyike.
Rais Tenga amewaomba radhi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na uamuzi huo
wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na mkutano huo mpaka hapo watakapopewa
taarifa nyingi.
Amesema TFF inakaribisha kwa
mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo ambacho cha juu kimpira
duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kila mhusika katika
mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake.
“Nia yetu ni kuona watu
wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo wahusika
(waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA wakifika
wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko
yaliyotolewa,” alisema Tenga.
Rais Tenga amesema timu hiyo ya
FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga izungumze na nani kwa wakati gani,
hivyo ni vizuri waathirika na vyombo vyote vilivyohusika na mchakato wa
uchaguzi wakajiandaa.
Amesema ilikuwa ni muhimu suala
hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi
utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo kimoja badala ya kurudi katika
migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka tubakie kama tulivyokuwa.
Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA
ni chombo cha juu, nafurahi wamekubali kuingia katika hili, kwani wana shughuli
nyingi wangeweza kukataa,” amesema.
Kuhusu fursa ya kufanya marejeo
(review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inayoongozwa na Idd Mtiginjola
ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga amesema kwa vile hicho ndicho chombo cha
mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya
review.
“Kwa vile hakuna chombo kingine,
nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika utaratibu wa kutoa haki,
uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu. Nilidhani hilo linawezekana,
kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,”
amesema Rais Tenga.
Kamati ya Mtiginjola iliyokutana
jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya review yaliyowasilishwa mbele
yake na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna kipengele chochote kwenye
Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi kinachotoa fursa hiyo.
Waombaji hao walikuwa Jamal Emil
Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye
kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine ni walioomba kuwania
ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano; Eliud Peter
Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha
Matutu (Shinyanga na Simiyu).
0 comments:
Post a Comment