LYON KUJUA
MUSTAKABALI WAKE CHAMAZI
HATMA ya
African Lyon kuendelea kushika mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inajulikana kesho wakati itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja
Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Lyon yenye
pointi 13 kutokana na mechi 19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka
kuirejesha mkiani Toto African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi
zote tatu itabidi ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha
Charles Boniface Mkwasa.
Hiyo itakuwa
mechi ya 18 kwa Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26
ikitanguliwa na vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera
Sugar na Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa
Stars, Mecky Maxime.
Mechi hiyo
namba 139 itachezeshwa na mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni
Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani
atakuwa Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.
Nayo
Tanzania Prisons ya Jumanne Chale itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi
itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo
Shooting itaoneshana kazi na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
Keshokutwa
(Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa
mwenyeji wa mechi kati ya JKT Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.
Ligi hiyo
itaendelea tena Jumamosi ya Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto
Africans (Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).
TFF
YAWASILISHA RASMI MAOMBI KUMUONA WAZIRI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili
kuzungumzia uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.
Maombi hayo
yaliwasilishwa rasmi Wizarani jana (Machi 4 mwaka huu) ambapo TFF imependekeza
kikao hicho kifanyike keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.
Kamati ya
Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua
matumizi ya Katiba ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la
kusikiliza upande wa TFF katika suala hilo.
0 comments:
Post a Comment