HAYA NI YA TFF YA LEO




LYON KUJUA MUSTAKABALI WAKE CHAMAZI
HATMA ya African Lyon kuendelea kushika mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inajulikana kesho wakati itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Lyon yenye pointi 13 kutokana na mechi 19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka kuirejesha mkiani Toto African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi zote tatu itabidi ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha Charles Boniface Mkwasa.

Hiyo itakuwa mechi ya 18 kwa Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 ikitanguliwa na vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.

Mechi hiyo namba 139 itachezeshwa na mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.

Nayo Tanzania Prisons ya Jumanne Chale itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo Shooting itaoneshana kazi na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya JKT Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.

Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi ya Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).


TFF YAWASILISHA RASMI MAOMBI KUMUONA WAZIRI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili kuzungumzia uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.

Maombi hayo yaliwasilishwa rasmi Wizarani jana (Machi 4 mwaka huu) ambapo TFF imependekeza kikao hicho kifanyike keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.

Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua matumizi ya Katiba ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la kusikiliza upande wa TFF katika suala hilo.

HAYA NI YA TFF HII LEO.

FIFA YAWASILISHA MAREKEBISHO 10 YA KATIBA KWA WARAKA
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limetuma mapendekezo 10 ya marekebisho ya Katiba yake kwa wanachama wake kwa njia ya waraka.

Mapendekezo hayo yametumwa kwa kila nchi mwanachama kupitia waraka namba 1320, ambapo wanachama kwa kupitia kwa mashirikisho yao ya mabara watapiga kura ya ndiyo au hapa. Kwa upande wa Afrika, wanachama wa FIFA wanatakiwa kuwasilisha kura zao kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Baadhi ya mapendekezo hayo ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa FIFA (FIFA Congress). Makamu wa Rais wa FIFA na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaochaguliwa katika mabara ambapo itabidi wathibitishwe na FIFA Congress.

Muundo wa Kamati ya Utendaji; nafasi moja ya vyama vya mpira wa miguu vya Uingereza (British FAs) sasa inahamishiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA). Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya FIFA anatakiwa kushiriki vikao vya Kamati ya Utendaji bila kuwa na haki ya kupiga kura.

Uchaguzi wa Rais; mgombea anatakiwa kuungwa mkono na idadi ya kutosha ya vyama wanachama kutoka katika mabara mawili tofauti. Ukomo wa uongozi; kuanzisha vipindi vya uongozi. Ukomo wa umri; ukomo wa umri usiozidi miaka 72 wakati wa kugombea utekelezwe.

Uwakilishi wa kutosha kwa makundi yenye maslahi katika FIFA; makundi yenye maslahi katika mpira wa miguu kama wachezaji wapate uwakilishi katika Kamati ya Mpira wa Miguu. Uteuzi wa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia; uteuzi sasa ufanywe na Mkutano Mkuu wa TFF.

WATAZAMAJI 13,398 WAZISHUHUDIA YANGA, KAGERA
Watazamaji 13,398 wameshuhudia pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Kagera Sugar lililochezwa juzi (Februari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 77,117,000.

Mechi hiyo namba 130 iliyochezeshwa na Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ilimalizika kwa Yanga ambao wanaongoza VPL wakiwa na pointi 42 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 45 na Haruna Niyonzima.

Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 18,291,297.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,763,610.17.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 11,908 na kuingiza sh. 59,540,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 80 na kuingiza sh. 1,600,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 9,300,659.97, tiketi sh. 3,348,990, gharama za mechi sh. 5,580,395.98, Kamati ya Ligi sh. 5,580,395.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,790,197.99 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,170,153.99.

POLISI KUIKABILI OLJORO KUNG’ANG’ANIA VPL
Polisi Morogoro inaikaribisha Oljoro JKT ya Arusha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mechi pekee ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itakayochezwa kesho (Machi 2 mwaka huu).

Hata hivyo, timu hizo haziko katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa ambapo Yanga ndiyo inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 42 wakati Oljoro JKT inayofunzwa na Alex Mwamgaya ikiwa nazo 21 na Polisi Morogoro pointi 15.

Oljoro JKT iko katika nafasi ya tisa. Polisi Morogoro ambayo katika mzunguko wa pili imebadilika ikiwa chini ya Kocha Adolf Rishard inashika nafasi ya 12 ikiziacha mkiani Toto Africans yenye pointi 14 na African Lyon ambayo ina pointi 13.

Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Machi 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Oljoro JKT vs Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid), African Lyon vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Chamazi) na Mgambo Shooting vs Mtibwa Sugar (Mkwakwani) wakati Machi 7 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Kagera Sugar (Azam Complex, Chamazi).

Machi 9 mwaka huu kutakuwa na mechi mbili; Yanga vs Toto Africans 9Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).

VILLA SQUAD KUIVAA ASHANTI UNITED FDL
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Machi 2 mwaka huu) katika makundi yote matatu. Villa Squad itaivaa Ashanti United kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B.

Kundi A ni mechi kati ya Kurugenzi ya Mafinga dhidi ya Mbeya City wakati Polisi Iringa vs JKT Mlale, na Majimaji vs Mkamba Rangers zilizokuwa zicheze kesho (Machi 2 mwaka huu), sasa zitaumana Machi 3 mwaka huu mjini Iringa na mjini Songea.

Pia kundi B kesho (Machi 2 mwaka huu) ni Green Warriors vs Transit Camp (Mlandizi) wakati keshokutwa (Machi 3 mwaka huu) Polisi Dar vs Tessema (Karume) na Ndanda vs Moro United katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi za kundi C kesho ni JKT Kanembwa vs Polisi Tabora (Lake Tanganyika), Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Karume, Musoma), Morani vs Pamba (Kiteto) na Mwadui vs Rhino Rangers (Kambarage, Shinyanga).

SIMBA KUONDOKA NCHINI KESHO

KIKOSI kamili cha Simba kinaondoka jijini Dar es Salaam kesho kikiwa na msafara wa watu 18, wakiwamo wachezaji 18 na viongozi saba.
 
Wachezaji wanaoondoka ni Juma Kaseja, Abel Dhaira, Nassor Said Masoud, Amir Maftah, Koman Bili Keita, Juma Nyoso, Shomari Kapombe, Salim Kinje, Ramadhani Chomboh, Amri Kiemba, Haruna Moshi, Kiggi Makasi, Abdallah Seseme, Amri Kiemba, Haruni Chanongo, Mrisho Ngassa, Felix Sunzu na Abdallah Juma.
 
Viongozi ni Zacharia Hans Poppe, Muhsin Balhabou, Patrick Liewig, Jamhuri Kihwelo, Dk. Cosmas Kapinga, James Kisaka na Kessy Rajab.
 
Simba inaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) majira ya saa 11:10 alfajiri na inatarajiwa kufika Luanda, Angola majira ya saa nne asubuhi.
 
Timu itafanya mazoezi ya mwisho jijini Dar es Salaam leo jioni kabla ya kuelekea kambini ambapo wachezaji watapumzika kusubiri muda wa safari.
 
Mechi kati ya Simba na Libolo itachezwa Machi 3 (Jumapili ijayo) katika Uwanja wa Calulo uliopo katika mji wa Calulo jimbo la Kwanza Sul (Kwanza Kusini).